Wakulima Moro watumia mbegu za soya kuzalisha maziwa

MOROGORO: WAKULIMA wa vijiji vinne vya Mkoa wa Morogoro wameanzisha miradi ya uchakataji maziwa yanayotokana na mbegu za soya kwa lengo la kuongeza wigo mpana unywaji maziwa kwenye jamii na kwa wanafunzi wa shule za msingi. Mratibu wa Mradi wa Ushirikiano kati ya Mkoa wa Morogoro na Chuo Kikuu cha Kilimo cha China, Waziri Mahimbo …
MOROGORO: WAKULIMA wa vijiji vinne vya Mkoa wa Morogoro wameanzisha miradi ya uchakataji maziwa yanayotokana na mbegu za soya kwa lengo la kuongeza wigo mpana unywaji maziwa kwenye jamii na kwa wanafunzi wa shule za msingi.
Mratibu wa Mradi wa Ushirikiano kati ya Mkoa wa Morogoro na Chuo Kikuu cha Kilimo cha China, Waziri Mahimbo amesema hayo kwenye banda la Wasimba Soya Farmers Group walioshiriki maadhimisho ya Wiki ya Maziwa Kitaifa mkoani Morogoro.
Mahimbo amesema utekelezaji huo unaendana na uzalishaji wa zao la soya kwenye vijiji hivyo vinne ambavyo ni Mtego wa Simba cha Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, Peapea na Kitete vya Wilaya ya Kilosa, na kijiji cha Makuyu wilayani Mvomero.
“Kilimo cha zao hili na uendeshaji mradi wa maziwa yatokanayo na mbegu za soya unatekelezwa na vikundi vya wakulima ,lengo kubwa ni kuboresha afya za wananchi kutokana na unywaji wa maziwa na uuzaji wa soya kuinua vipato vyao,” amesema Mahimbo.
Naye Ofisa Ugani wa kijiji cha Mtego wa Simba , kata ya Mikese ,halmashauri ya wilaya ya Morogoro,Veronica Lugano amesema wakulima wa kijiji hicho ni wazalishaji wazuri wa zao hilo ambapo wastani huzalisha tani 2.5 kwa mwaka.
Lugano amesema licha ya kuuza zao hilo kwenye masoko, pia wakulima wameazisha mradi wa utengenezaji maziwa ya soya.
“Sifa kubwa ya zao hili lina viini lishe aina ya protini kwa wingi kuliko zao lingine lolote la jamii ya mikunde ,inakadiriwa kuwa na asilimia 35 hadi 40 ya soya ni protini,” amesema Lugano.
Lugano amesema soya inaweza kutumika kama chakula ,kutengeneza maziwa mafuta ya kupikia, chakula cha mifugo na masalia yatokanayo na zao hilo yanaweza kutumika kurutubisha udongo.
“Maziwa ya soya ni kinywaji kizuri kwa afya na pia hutumika kama kiburudisho na hufanana na maziwa ya wanyama hasa ya ng’ombe katika virutubisho na pia mwonekano wa rangi,” amesema Lugano.
Lugano amesema mradi wa maziwa ya soya unaotekelezwa utachangia kuboresha afya za familia hasa zile zinazoishi maeneo ambayo upatikanaji wa maziwa ya ng’ombe ni wa shida.
Amesemakuwa muhula ujazo wa masomo, mradi huo utawezesha utoaji maziwa ya soya kwa wanafunzi zaidi ya 350 wa shule ya Msingi Juhudi iliyopo katika kijiji hicho.
SOMA ZAIDI
Wakulima kupewa elimu kilimo tija
Kwa upande wake Katibu wa Kikundi hicho ,Shomari Jaeka amesema kina wakulima zaidi ya 25 na kiliazishwa mwaka 2023 baada ya kuwepo kwa Ushirikiano kati ya Mkoa wa Morogoro na Chuo Kikuu cha Kilimo cha China.
Kwa mujibu wa Bodi ya MaziwaTanzania (TDB),katika maadhimisho ya wiki ya Maziwa kifaifa yam waka huu yaliyofanyika Morogoro ,uzalishaji wa maziwa mwaka 2024/2025 ni lita bilioni 4.01, wakati unywaji maziwa kwa kipindi hicho ni lita 68.1 kwa mtu kwa mwaka .