Viongozi Chadema waliohamia Chaumma wakana kununuliwa

Habari Leo
Published: Jun 05, 2025 07:00:09 EAT   |  News

VIONGOZI waliotoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na kuhamia Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA) wamekanusha tuhuma za kununuliwa wakidai kwamba wanapigania haki na demokrasia nchini. Wakizungumza kwenye uzinduzi wa Operesheni ya Chaumma for Change (C4C) kwenye Viwanja vya Furahisha jijini Mwanza walisema wao si wanachama wa chama ambacho kimenunuliwa. Katibu Mkuu wa chama …

VIONGOZI waliotoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na kuhamia Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA) wamekanusha tuhuma za kununuliwa wakidai kwamba wanapigania haki na demokrasia nchini.

Wakizungumza kwenye uzinduzi wa Operesheni ya Chaumma for Change (C4C) kwenye Viwanja vya Furahisha jijini Mwanza walisema wao si wanachama wa chama ambacho kimenunuliwa.

Katibu Mkuu wa chama hicho, Salum Mwalimu alisema yeye na maelfu na waliokuwa wanachama wa Chadema wameamua kuachana na ulaghai, mipango dhalimu ya kuua demokrasia, kulinda na kuheshimu nguvu kubwa ya kujenga demokrasia na upinzani nchini.

Alisema wataendelea kupinga udhalimu huo na kwamba Watanzania wataelewa kinachoendelea nyumba ya jirani siku si nyingi na kwamba waliohamia Chaumma ni vichwa na wamejenga misingi ya kupigania haki na demokrasia ya nchi.

“Nina miaka 20 ya jasho na damu, kupigania haki yangu, nimehatarisha maisha, fursa nyingi zimenikataa tangu nikiwa mwandishi wa habari Channel Ten, watu waliokaribu nami wanajua na wametumia mbinu zote kunishawishi lakini nikaamua kusimamia haki na demokrasia,’’ alisema Mwalimu.

Alisema aliweka ahadi ya kupigania maisha ya Watanzania kama walivyomlea bila baba yake, aliyefariki akiwa na miaka mitatu na akakua, akasoma na kuwa mtu wa maana.

“Halafu kuna mtu anakuja anasema umenunuliwa, aah! Bei gani, bei gani Salum Mwalimu nimenunuliwa? Wawaambie nimenunuliwa bei gani? Mbona hawasemi?’’ alihoji.

Mwalimu alisema, “tumekataa usanii wa kisiasa, dhuluma, utapeli wa kisiasa, tumesema tutawasimamia Watanzania na mtuite majina yote lakini kitaeleweka Oktoba, tutawasemea Watanzania na mtatuelewa.”

Alieleza kuwa alikuwa kiongozi wa kwanza kuswekwa siku 16 gerezani na kwamba baada ya kutoka aliulizwa kama atarudia na kueleza hatokata tamaa.

“Nimeshindwa kununuliwa nikiwa kijana mdogo, nimeahidiwa vyeo na kupigwa biti tusitangaze habari za upinzani, nilisema nitatangaza, walinitishia kunifukuza kazi nikasema nifukuzeni. Nilisimamishwa kufanya mitihani yangu ya mwaka wa tatu kisa kupigania demokrasia ya Tanzania, sikuomba radhi na sikurudi nyuma,’’ alisisitiza.

Alisema watasema kwa maneno na matendo na kuwasimamia Watanzania kama walivyofanya na kupoteza fursa, mali na kila bahati ambayo waliipata na kusisitiza waache waitwe majina wanayotaka na hawatorudi nyuma.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu Chaumma, Kigaia Benson alisema chama hicho hakijanunuliwa na Chama  Cha Mapinduzi (CCM) ili kiwapinge na badala yake wataenda nao sambamba ili wasipite bila kupingwa.

“Chama kinachosusia uchaguzi na kuruhusu CCM ipite bila kupingwa na kile kinachokwenda kushiriki uchaguzi kipi kimenunuliwa. Akili za kuambiwa changanya na za kwako,’’ alisema.

Alisema malengo ya vyama vya siasa ni kuchukua dola na njia ya kufikia malengo hayo ni kushiriki kwenye uchaguzi.