Tanzania yapiga hatua kizazi usawa wa kijinsia

DAR ES SALAAM: TANZANIA imepiga hatua katika kuimarisha kizazi chenye usawa wa kijinsia katika masuala ya kiuchumi, majukwaa, kisayansi, masuala ya ubunifu, ujumuishi wa sekta ya fedha na mikopo ya serikali za mitaa. Sio hivyo tu, pia haki za wanawake, wanaume na vijana katika kupata haki, kumiliki na kuitumia ardhi kwa rasilimali ya uzalishaji pia …
DAR ES SALAAM: TANZANIA imepiga hatua katika kuimarisha kizazi chenye usawa wa kijinsia katika masuala ya kiuchumi, majukwaa, kisayansi, masuala ya ubunifu, ujumuishi wa sekta ya fedha na mikopo ya serikali za mitaa.
Sio hivyo tu, pia haki za wanawake, wanaume na vijana katika kupata haki, kumiliki na kuitumia ardhi kwa rasilimali ya uzalishaji pia juhudi zimefanyika.
Mwenyekiti wa Kamati ya Ushauri ya Utekelezaji wa Programu ya Kizazi chenye Usawa, Angelah Kairuki ameeleza hayo jijini Dar es Salaam leo Juni 3, 2025 alipozungumza katika jukwaa la wadau wa habari wakiwemo wahariri wa vyombo vya habari ambapo amesema kuwa Watanzania wote wana haki sawa kupata, kumiliki kutumia na kuiendeleza ardhi.
“Katika mabadiliko ya kisera na kisheria, katika maandalizi ya bajeti mmeona zina mirengo ya kijinsia, ukiangalia Wizara ya Kilimo inazingatia masuala ya kijinsia, ukiangalia upatikanaji wa viuatilifu haijabagua,” amesema Kairuki.
Akizungumzia utekelezaji wa programu hiyo, Kairuki amewashauri wahariri wa vyombo vya habari kuwa programu hiyo inatekelezwa Tanzania Bara na Zanzibar, hivyo wanapaswa kuhakikisha wanapopata taarifa za Kizazi Chenye Usawa wanazifanyia kazi kwa ukubwa na ufanisi unaolingana.
Wajifungia kujadili usawa wa kijinsia
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Felister Mdemu ameviomba vyombo hivyo kutoa elimu kwa jamii kuhusu utekelezaji wa Programu ya Kizazi Chenye Usawa ili kuwezesha usawa wa kijinsia akiamini nguvu yake inaweza kufikisha ujumbe kwa wakati.
Amevitaja vyombo hivyo kuwa ni wadau wakubwa katika kuhakikisha taarifa za utekelezaji wa programu hiyo zinawafika kwa walengwa na kuongeza kuwa wahariri ni kundi ambalo linafikia jamii kwa haraka na kubadilisha fikra na mitazamo.
“Niseme tu ninyi ni muhimu katika kufikisha masuala mbalimbali katika jamii tulibebe na hili la usawa wa kijinsia tukaielimishe jamii ila kufikia malengo ya kuwa na Kizazi chenye usawa nchini,” amesema Mdemu.
Akizungumza katika kikao hicho, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri, Deodatus Balile amesema Jukwaa litahakikisha utekelezaji wa Programu hiyo kupitia vyombo vya habari linafanyika ili kuonesha uwepo wa usawa wa kijinsia katika jamii.
Watakiwa kuongeza uelewa usawa wa kijinsia
Naye Naibu Mwakilishi Mkazi UN Women Katherine Gifford amesema wataendelea kushirikiana na Serikali na wadau mbalimbali kuhakikisha agenda ya Kizazi Chenye Usawa inaeleweka na kuwafikia wananchi, ili kufikia azma ya kuwa na Kizazi Chenye Usawa Tanzania.
Mdau wa habari ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA) Joyce Shebe amesema kuna haja na umuhimu kuwekeza nguvu kwenye habari kuwaripoti wanawake walau kwenye kila habari.