Simulizi ya uchungu ya Albert Ojwang ambaye mauaji yake yamezua ghadhabu

"YUKO salama mikononi mwetu”.
Haya ndiyo maneno ya mwisho familia ya Albert Omondi Ojwang’ ilisikia kutoka kwa afisa wa polisi anayehudumu katika Kituo cha Polisi cha Mawego, Rachuonyo Kaskazini Jumamosi iliyopita.
Kinachosikitisha kuwa saa 24 baadaye mwalimu huyo mwenye umri wa miaka 27 alikuwa amefariki, mwili wake ukiwa umevimba na una damu. Iliripotiwa na polisi kuwa alikuwa amejitia kitanzi Nairobi, kilomita 320 kutoka nyumbani kwake.
Polisi huyo ambaye alikuwa kati ya polisi sita ambao walimweka Bw Ojwang’ kizuizini, aliwahakikishia kuwa angefikishwa mahakamani na hata kuachiliwa huru. Kauli hii iliipa familia hiyo wingu la matumaini na faraja
Hata hivyo, walisikitika na kutamauka waliposikia mwalimu huyo wa Kiswahili na Dini alikuwa ameaga dunia mikononi mwa polisi Nairobi.
Mnamo Jumanne, watu sita ambao walijitambulisha kama maafisa wa polisi walifika katika familia ya babake marehemu kwenye kijiji cha Kakoth, Lokesheni ya Kokwanyo wakiwa kwenye pikipiki tatu.
“Wawili waliingia kupitia ua wa nyuma kisha wa tatu akatumia lango la mbele. Wengine walizingira boma kana kwamba hawakuwa wakitaka mtu atoroke,” akasema Herman Ojwang’ mjomba wa marehemu.
Wakati huo familia hiyo ilikuwa imekusanyika kwa chakula cha mchana na walifikiria watu hao walikuwa wageni waliowatembelea.
Marehemu wakati huo hakuwa amejiunga na familia yake kwa kuwa alikuwa akikagua ujenzi uliokuwa ukiendelea wa nyumba yake.
Asubuhi hiyo alikuwa amenunua mbegu, akafanya kazi kwenye shamba lake ambalo alikusudia kupanda mboga.
Kabla kukamatwa, alikuwa amerejea nyumbani na mkewe alikuwa akijiandaa kumpa chakula chini ya mti, polisi hao walipofika.
“Tuliwaambia waingie ndani ya nyumba lakini wakakataa wakisema walikuwa wakimtafuta Ojwang," akasema Bw Opiyo.
Polisi hao waliambia familia hiyo alikuwa akisakwa kutokana na chapisho kwenye ukurasa wake wa X lililomtuhumu afisa mmoja wa ngazi ya juu kwenye idara ya polisi kwa kushiriki ufisadi.
Bw Ojwang’ alikamatwa, akatiwa pingu na kusafirishwa kwa pikipiki hadi kituo cha polisi cha Mawego. Kwa mujibu wa Bw Opiyo, familia yake ilimfuata lakini haikujua angesafirishwa hadi Nairobi na simu yake pia ilichukuliwa.
Polisi kituoni walimpa Bw Ojwang’ stakabadhi ya kurasa mbili ili aitie saini, akafanya hivyo kisha akaandika jina lake na nambari ya kitambulisho.
Hata hivyo, familia yake haikuruhusiwa kusoma stakabadhi hiyo na hakukuwa na idhibati maelezo kumhusu yalikuwa yamenakiliwa kituoni humo.
Baadaye Bw Opiyo alitumwa nyumbani amletee Bw Ojwang’ jaketi afisa mmoja akisema Nairobi kuna baridi na atahitaji nguo hiyo.
Polisi hao sita walimweka Bw Ojwang’ kwenye gari nyeusi lenye nambari ya kibinafsi kisha wakaondoka na wakaihakikishia familia kuwa mwanao yupo salama.
Babake marehemu, Bw Meshack Opiyo jioni hiyo aliabiri gari la kuelekea Nairobi lakini hata kabla kufika familia ilipokea habari Bw Ojwang’ alikuwa amekufa.
Taifa Leo ilipotembelea kituo cha polisi cha Mawego hakuna afisa ambaye alikuwa tayari kuongea huku wengi wao wakijificha.
Familia yake sasa inamwomba Katibu katika Wizara ya Usalama wa Ndani Dkt Raymond Omollo ahakikishe wanapata haki kuhusu mauti tata ya mwanao.
Bw Ojwang’, 27 mtoto wa pekee kwao alihitimu kutoka Chuo Kikuu cha Pwani mnamo 2022 na alikuwa akifundisha Voi akisubiri kupata kazi na serikali ikizingatiwa tayari alikuwa na nambari ya Tume ya Kuwaajiri Walimu Nchini (TSC).
“Nilijizatiti kumwelimisha mwanangu ili ainue maisha ya familia hii lakini sasa ameenda,” akasema Mamake Eucabeth Adhiambo huku akitiririkwa na machozi.
Mjombake mwengine Joseph Omumu alikashifu jinsi mauti yake yalivyotokea.
“Hatupingi kuwa alitoa madai kuhusu afisa lakini kile tulitaka ni mchakato wa kisheria kufuatwa. Hangeuawa,” akasema Bw Omumu.
Familia hiyo pia ilisema marehemu hakuwa na historia ya kuugua maradhi yoyote au hata tatizo la kiakili na wamepinga kauli ya polisi kuwa alijigonga kwenye ukuta wa seli.