Seneti yahoji ujenzi wa makazi ya gavana utakaomeza Sh300 milioni ilhali miradi imekwama

Taifa Leo
Published: Jun 05, 2025 04:55:37 EAT   |  Business

KAUNTI ya Kwale imemulikwa kuhusu mradi wa kujenga makazi ya gavana ambao umedumu kwa karibu mwongo mmoja licha ya kumiminiwa mamilioni huku serikali ya kaunti ikilaumu mdhibiti wa bajeti kwa ucheleweshaji huo. Gavana Fatuma Achani alieleza Kamati ya Seneti kuhusu Ukaguzi wa Hesabu za Umma (CPAC) katika kikao Jumanne kuwa mradi huo unaendelea na unatarajiwa kukamilika mwaka ujao, Machi 2026, kiasi cha jumla kikikadiriwa kufikia zaidi ya Sh300 milioni. Kamati hiyo inayoongozwa na Seneta wa Homa Bay, Moses Kajwang, ilihoji sababu ya ujenzi wa makazi ya gavana ulioanzishwa wakati wa hatamu ya Bw Salim Mvurya aliyekuwa gavana wa kwanza Kwale, umegharimu kiasi hicho cha pesa na kwa nini bado haujakamilika. Mradi huo kufikia sasa umegharimu jumla ya Sh119 milioni tangu serikali ya kaunti ilipotia saini kandarasi ya kuanzisha ujenzi wa makazi ya gavana yenye thamani ya Sh149 milioni katika muda wa mwaka mmoja. Agosti 2019, muda wa kandarasi hiyo uliongezwa kwa nyongeza ya Sh3.6 milioni lakini bado haukukamilika ambapo sasa mwanakandarasi anadai kaunti Sh27 milioni kwa kupotezewa muda na kucheleweshwa, Seneti iliambiwa. “Huku tukiendelea na ‘kizungu mingi’ makazi ya gavana bado hayajakamilika. Mwanakandarasi kufikia sasa amelipwa 119 milioni ilihali ikulu ndogo Kwale na Homabay zilijengwa kwa miezi mitatu tu,” alisema Seneta Kajwang. Hata hivyo, Afisa Mkuu, Thomas Onduko, alieleza Kamati ujenzi unaendelea na mradi huo “umekamilika asilimia 64 kulingana na ukaguzi wa miradi ya umma” na unatazamiwa kugharimu “Sh240 milioni ikiwemo Sh27 milioni za ziada.” “Baada ya kumlipa Sh3 milioni, mwanakandarasi alitoweka. Tulimpa notisi mara mbili inavyohitajika kisheria kabla ya kukatiza kandarasi. Sasa anadai kupotezewa muda na mashine zake kukaa bila kufanya kazi lakini hajathibitisha alipoteza fursa kwa sababu ya mashine zake kuwepo kwenye eneo la mradi wetu,” alifafanua. Kuhusu mradi huo kujikokota, alilaumu mdhibiti wa fedha (CoB) kwa kuchelewesha fedha kuwezesha kukamilishwa kwa muda uliopangiwa. “Tulichelewa kwa sababu ya mapendekezo yaliyotolewa na seneti. Ilituchukua karibu miaka miwili kwa CoB kuachilia fedha, Hii ilikuwa kabla ya muafaka wa seneti.” Seneti ilihoji kwa nini makazi ya gavana yamegharimu kiasi hicho ilhali miradi mingineyo bado haijakamilika ikiwemo soko la Kombani na kiwanda cha chakula na kumwagiza usimamizi wa kaunti kuangazia upya kiasi hicho. “Kama mnang’ang’ana kujenga kiwanda cha chakula chenye thamani hamfai kuwa mnatumia pesa kama hizi. Mradi huu una thamani ikiwa masoko yenu yanafanya kazi,” alisema Mwenyekiti. “Ni uovu kwa kaunti kutumia kiasi hicho cha pesa huku ikiwa imeshindwa kutimiza malengo yake ya mapato ya kibinafsi yanayokusanywa. Ni haki kukusanya pesa za leseni na ada kujenga kasri la gavana? Angazieni upya na mkamilishe kwa kiasi cha chini.” Gavana Achani alisema amewaagiza wahandisi kuangazia upya mradi huo huku suala hilo likizidi kutatuliwa. Mwaka wa 2019, Seneti iliafikiana kudhibiti kiasi cha fedha zinazotumika kujenga makazi ya wakuu wa kaunti yasipite Sh45 milioni kwa makao ya gavana, Sh35 milioni naibu gavana na ya spika.