Sekta ya usafirishaji yapaa, ofisi ya kanda ikizinduliwa Iringa

Habari Leo
Published: Jun 02, 2025 10:09:06 EAT   |  Educational

IRINGA: Sekta ya usafirishaji nchini imezidi kupata mwelekeo mpya baada ya Chama cha Wasafirishaji Tanzania (TAT) kuzindua rasmi ofisi yake ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini mjini Iringa, tukio lililoambatana na mkutano wa mwaka wa usafiri na usafirishaji uliowakutanisha wadau muhimu serikalini na binafsi. Uzinduzi huo uliambatana na utoaji wa elimu kwa wanachama na …

IRINGA: Sekta ya usafirishaji nchini imezidi kupata mwelekeo mpya baada ya Chama cha Wasafirishaji Tanzania (TAT) kuzindua rasmi ofisi yake ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini mjini Iringa, tukio lililoambatana na mkutano wa mwaka wa usafiri na usafirishaji uliowakutanisha wadau muhimu serikalini na binafsi.

Uzinduzi huo uliambatana na utoaji wa elimu kwa wanachama na wadau kutoka taasisi mbalimbali kama TANROADS, TARURA, Wakala wa Vipimo, AIR Tanzania, TRA, RATRA na taasisi za kifedha, jambo lililodhihirisha mshikamano wa pamoja wa kukuza sekta hiyo muhimu kwa maendeleo ya uchumi wa taifa.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo kwa niaba ya Naibu Waziri wa Uchukuzi David Kihenzile, Mkuu wa Wilaya ya Iringa Kheri James alisema kuwa serikali inatambua mchango mkubwa wa wasafirishaji na kwamba ipo tayari kushirikiana nao katika kuboresha mazingira ya utendaji kazi.

“Niwahakikishie kuwa tutafanya kazi bila kuchoka kushughulikia changamoto za sekta hii na wadau wake. Serikali inapendekeza mkutano wa aina hii ufanyike kila mwaka ili kuimarisha sekta na kushughulikia changamoto zake kwa wakati,” alisema DC James.

SOMA ZAIDI

Vipaumbe usafiri, usafirishaji Ilani ya CCM 2025-2030

Kwa upande wake, Kaimu Rais wa Chama cha Wasafirishaji Tanzania, Omari Said Kiponza alisema kuwa chama hicho kilichoanzishwa mwaka 2015, kimekuwa kwa kasi na sasa kina wanachama zaidi ya 1,000.

“Chama hiki kinajumuisha wasafirishaji wa njia kuu, majini na angani, ambao ni wadogo wa kati na wakubwa. Kufungua ofisi hii ya kanda ni hatua kubwa ya kusogeza huduma karibu na wanachama wetu wa mikoa ya Iringa, Njombe, Mbeya na Songwe,” alisema.

Alisema wataendelea kufanya kazi kwa karibu na serikali na wadau kama TANROADS, TARURA, RATRA, Polisi na taasisi nyingine kuhakikisha mazingira bora ya utendaji.

Kupitia ofisi hiyo ya kanda, alisema wasafirishaji wataweza kupata huduma kwa urahisi zaidi, zikiwemo za ushauri, mafunzo, utetezi wa haki zao na uhusiano na mamlaka mbalimbali.

Wakati huo huo Mkuu wa Wilaya ya Iringa alisema katika kuimarisha huduma za usafirishaji na kupunguza msongamano wa magari makubwa katikati ya mji wa Iringa, serikali imeanza utekelezaji wa ujenzi wa barabara mbili muhimu kwa maendeleo ya kanda hiyo.

Mosi ni barabara ya lami ya Iringa – Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, ambayo inajengwa kwa kiwango cha juu na inatarajiwa kukamilika ndani ya miaka miwili.

Alisema barabara hiyo ni muhimu kwa kukuza utalii na uchumi kwa kuunganisha mji huo wa Iringa na vivutio vikubwa vya asili nchini.

Pili ni ujenzi wa barabara ya mchepuo ya Tumaini–Igumbilo, ambao umeshaanza na unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 12.

Alisema tayari miezi miwili imepita, na baada ya kukamilika, magari makubwa hayatapita tena katikati ya mji wa Iringa, hatua ambayo itaboresha usalama na mazingira ya wakazi wa mjini.

“Ni mageuzi makubwa ya sekta ya miundombinu tunayoshuhudia. Wananchi wa kanda hii waanze kufikiria huduma bora zaidi za usafiri na usafirishaji,” alisema James.

Katika mkutano huo, taasisi mbalimbali zilizotoa mchango mkubwa katika maendeleo ya sekta ya usafirishaji zilitunukiwa tuzo maalum, zikiwemo TANROADS, TARURA, TRA, Meya wa Iringa na AIR Tanzania.

Mkutano huo ulitoa pia nafasi kwa wadau kujadili changamoto na fursa zilizopo katika sekta ya usafirishaji, ikiwa ni pamoja na umuhimu wa bima, matumizi ya mizani, leseni na taratibu za kodi.