Raila akutana na Rais wa Somaliland aliyetengwa na maafisa wa Mudavadi

Taifa Leo
Published: Jun 03, 2025 11:07:23 EAT   |  News

BAADA ya kuepukwa wiki jana na maafisa wa Wizara ya Masuala ya Kigeni wa Kenya, Rais wa jimbo la Somaliland Abdirahman Mohamed Abdillahi Jumanne, Juni 3, 2025, alipata fursa ya kukutana na Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga. Kwenye taarifa fupi kupitia akaunti yake ya mtandao wa X, Bw Odinga alisema kuwa kiongozi huyo alimtembelea nyumbani kwake katika mtaa wa Karen, Nairobi. “Mama Ida na mimi tulikuwa wenyeji wa Rais wa Somaliland Mheshimiwa Dkt Abdirahman Mohamed Abdillahi (Ciro) nyumbani kwetu Karen, Nairobi,” Bw Odinga akasema. Aliongeza kuwa kiongozi huyo aliandamana na wanachama wa baraza lake la mawaziri na maafisa wa afisi ya kibalozi ya Somaliland Nairobi. Kulingana na taarifa hiyo, Rais Abdirahman alimwelezea Odinga “mzalendo na mmoja wa marafiki wa dhati wa jimbo la Somaliland”. “Tunakushukuru kwa kuunga mkono maono ya Somaliland ya kujipatia nafasi yake ya halisi miongoni mwa jamii ya kimataifa. Kujitolea kwako katika kufikiwa kwa umoja wa Afrika na maendeleo kunatupa shime,” kiongozi huyo akaongeza. Rais Abdillahi amemtembelea Bw Odinga, ambaye ni kiongozi wa ODM, siku kadhaa baada ya maafisa wa Wizara ya Masuala ya Kigeni nchini kujitenga kabisa la hafla ya kufunguliwa kwa Afisi Ndogo ya Kibalozi ya Somaliland jijini Nairobi Alhamisi wiki jana. Sherehe hiyo ya ufunguzi wa afisi hizo zilizoko mtaa wa Gigiri, Nairobi, zilihudhuriwa na Rais Abdillahi na maafisa wa serikali yake. Duru zilisema kuwa maafisa wa Kenya walisusia hafla hiyo ili kuzuia mgogoro wa kidiplomasia kati ya Kenya na Somalia ambayo ingali inadai kuwa jimbo la Somaliland liko ndani ya himaya yake. Lakini kinaya ni kwamba mnamo Ijumaa, Mei 30, 2025, Rais William Ruto mwenyewe alifanya mkutano na Rais Abdillahi katika Ikulu ya Nairobi ambapo ilisemekana kuwa wawili hao walijadili masuala ya kujenga uhusiano kati ya Kenya na Somaliland. “Mheshimiwa Abdirahman Mohamed Abdillahi, Rais wa Jamhuri ya Somaliland, alifanya mkutano wa kufana  na Rais William Ruto katika Ikulu ya Nairobi,” ikasema taarifa kutoka kwa Ikulu.