Orengo sasa akunja mkia, aelekea Ikulu kuomba miradi ya maendeleo

Taifa Leo
Published: Jun 05, 2025 06:55:41 EAT   |  News

GAVANA James Orengo ambaye alikuwa ametangaza kuwa hawezi kupiga magoti ili kupata miradi ya maendeleo anaonekana kubadilisha msimamo na Alhamisi Juni 5, 2025 anatarajiwa kuongoza ujumbe wa viongozi kutoka Siaya kuzuru Ikulu ili kuomba miradi katika kaunti yake.
 Hatua hiyo imefasiriwa kuwa kunyenyekea kwa mwanasiasa huyo mkakamavu ambaye alikuwa amesisitiza kuwa miradi kutoka serikali ya kitaifa ni haki ya kila eneo. Alikuwa amedai kuwa miradi hiyo haifai kutolewa baada ya wanasiasa ‘kumwabudu’ Rais. Bw Orengo amekuwa mmoja kati ya wanasiasa wakosoaji wakuu wa Rais Ruto na pia kuwashutumu wenzake kutoka ODM walio ndani ya Serikali Jumuishi akiwaita vibaraka. Kauli zake za kukosoa serikali zimemweka pabaya na baadhi ya viongozi wa ODM akiwemo Seneta wa Siaya Dkt Oburu Oginga na Waziri wa Kawi Opiyo Wandayi ambaye pia anatoka kaunti hiyo. Kwa mujibu wa Mbunge wa Bondo Gideon Ochanda, baadhi ya viongozi waliochaguliwa walikutana Nairobi kuhakiki orodha ya mwisho ya miradi ambayo watajadili na Rais Ikulu. Gavana naye aliandaa mkutano na Waziri wa Fedha John Mbadi ambapo walizungumzia miradi inayostahili kupewa kipaumbele kwenye bajeti kabla ya mkutano wa leo. “Niliandaa mazungumzo na Waziri John Mbadi kuhusu miradi ya kupewa kipaumbele Siaya kuelekea mkutano wa Alhamisi na Rais Ruto pamoja na viongozi wa Siaya,” Bw Orengo aliandika kwenye ukurusa wake wa Facebook. Jumatano hakupokea simu kufafanua zaidi kuhusu miradi hiyo na mkengeuko wake kutoka msimamo mkali alioushikilia hapo awali. Mwenyekiti wa kamati ya Bunge kuhusu Bajeti Sam Atandi (Mbunge wa Alego Usonga) alisema mkutano wa Ikulu umeandaliwa kutokana na kuingilia kati kwa Bw Wandayi. “Bado hatujasuluhisha masuala ya kisiasa na gavana lakini tumekubali kuungana na kusaka miradi ya serikali ya kitaifa,” akasema Bw Atandi. “Amekuwa (Orengo) akiwaita baadhi yetu vibaraka kwa kusaka miradi na kwa kuwa sasa ameungana nasi, tutaendelea kumkumbusha miradi inasakwa,” akaongeza. Mnamo Aprili 12, wakati wa mazishi ya mlinzi wa Raila Odinga, marehemu George Oduor, Bw Orengo alitoa matamshi makali dhidi ya serikali mbele ya Raila na Rais Ruto. “Nawaambia kuwa kibaraka hakitatupeleka mahali na mwaambieni kiongozi wenu ukweli. Mimi si kibaraka na nchi hii itasambaratika iwapo lugha ambayo nimesikia hapa itaendelea, “Kama kuna miradi ambayo inaletwa Siaya, ni haki wala si kwa sababu tunafanyiwa hisani,” akasema Bw Orengo. Siku chache baadaye, mnamo Aprili 17 kwa heshima kuu aliandika barua ya kuomba kuwe na mkutano wa mashauriano kati ya Rais na viongozi kutoka Siaya kuhusu miradi ya maendeleo Siaya. Kwenye barua hiyo, gavana huyo alisema viongozi wote waliochaguliwa kuanzia madiwani wangehudhuria mkutano huo pamoja na wale ambao wanahudumu katika serikali ya kitaifa na kaunti. Pia, alipendekeza kikao hicho kiandaliwe wiki ya mwisho ya Aprili akisema alikuwa na matumaini kingezaa umoja na pia kuwanufaisha wakazi wa Siaya kupitia miradi ya maendeleo
Ombi hilo lilikataliwa huku wandani wa Raila wakiendelea kumshambulia lakini Bw Odinga mwenyewe mara si moja alijitokeza kumtetea. Mapema Mei wakati Rais Ruto alikuwa ziarani Kaunti ya Migori, Dkt Oginga alimtaka Bw Orengo aondoke ODM iwapo anapinga Serikali Jumuishi. “Gavana wangu akisimama na kusema amekasirishwa, sijui na nani na anadai anataka kusema ukweli. Huwa najiuliza ukweli gani?
“Wale ambao wanahisi Serikali Jumuishi ni mbaya wanatutapikia wakiwa ndani. Mbona wasitoke nje na kututapikia wakiwa nje?” akauliza Dkt Oginga. Bw Orengo alichaguliwa kwa mara ya kwanza bungeni mnamo 1980 na amekuwa na uhusiano imara na pia vuguvugu na Bw Odinga. Baada ya kifo cha Jaramogi Oginga Odinga (babake Raila na Oburu), Raila na Orengo walizozania uongozi wa Ford Kenya na ubabe wa siasa za Luo Nyanza. Bw Orengo alikuwa mrengo wa Wamalwa Kijana ambaye alikuwa akiwania uenyekiti wa Ford Kenya dhidi ya Raila.
Licha ya Raila kubuni NDP, Bw Orengo alisalia Ford Kenya na hata akafaulu kutetea kiti chake kupitia chama hicho 1997. Hii ni licha ya kwamba, kulikuwa na mawimbi ya NDP Nyanza wakati huo.
Mnamo 2002, Bw Orengo aliwania urais kupitia SDP lakini akapoteza ubunge pamoja na urais huku Mwai Kibaki aliyekuwa akipigiwa upato na Raila Odinga akishinda. Kiti cha Ugenya kilinyakulia na Askofu Stephen Ondiek aliyewania kupitia Narc na aliegemea mrengo wa LDP wa Bw Odinga. Hata hivyo, wanasiasa hawa wawili walirudiana 2007 huku Bw Orengo akishinda ubunge tena na kuteuliwa waziri ndani ya serikali ya muungano. Ameishia kuwa seneta wa Siaya kwa mihula miwili kabla ya kushinda ugavana 2022.