Mpango aonya kufuata mkumbo kampeni za vurugu

Habari Leo
Published: Jun 05, 2025 04:48:57 EAT   |  News

SERIKALI imetoa mwito kwa Watanzania wasiingie kwenye mkumbo wa kufanya kampeni za vurugu au kutukanana kwa kuwa si jadi ya Mtanzania. Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango amesema hayo Arusha kwenye mkutano Mkuu wa 55 na Kongamano la Kisayansi la Mwaka la Chama cha Wafamasia Tanzania (PST). Dk Mpango amehimiza Watanzania washiriki Uchaguzi Mkuu kwa …

SERIKALI imetoa mwito kwa Watanzania wasiingie kwenye mkumbo wa kufanya kampeni za vurugu au kutukanana kwa kuwa si jadi ya Mtanzania.

Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango amesema hayo Arusha kwenye mkutano Mkuu wa 55 na Kongamano la Kisayansi la Mwaka la Chama cha Wafamasia Tanzania (PST).

Dk Mpango amehimiza Watanzania washiriki Uchaguzi Mkuu kwa amani, wasifanye vurugu na kuhatarisha amani na wachague viongozi sahihi na si wachumia tumbo.

“Hakikisheni mnaboresha taarifa zenu za mpigakura ili siku ya uchaguzi tukapige kura, lakini nawaomba na kuwasihi mkaziambie familia zenu, marafiki na majirani tusiingie kwenye mkumbo wa kufanya kampeni za vurugu, za kutukanana kwani sio jadi ya Mtanzania,” alieleza Dk Mpango.

Alisema na Mungu asimamie wapatikane viongozi watakaosimamia maslahi ya Mama Tanzania hivyo uchaguzi wa amani ndiyo njia pekee ambayo imekubalika ya kuingiza viongozi madarakani na wawe viongozi bora na si viongozi wachumia tumbo.

Alisema viongozi watakaochaguliwa wawe ni viongozi watakaolinda amani ya Tanzania kwani bila amani itakuwa vigumu kufanya shughuli zozote za kujiletea maendeleo.

Aidha, alisema serikali itaendelea kushirikiana na wafamasia kuhakikisha utoaji huduma bora unaimarika na kuongeza kuwa kumekuwepo na matumizi ya dawa yasiyo rasmi ikiwamo dawa kutumika kama kilevi, matumizi ya dawa kunenepesha mifugo ikiwamo kukoleza pombe za asili.

“Toeni kipaumbele katika matumizi sahihi ya dawa ili kusaidia ikiwemo utafiti wa matumizi ya tafiti za dawa kwani nchi yetu ina uoto wa asili wa aina mbalimbali za mimea hivyo Tamisemi tengeni maeneo kwenye halmashauri mbalimbali nchini ili miti dawa ipandwe kwa ajili ya kufanya tafiti,” alieleza Dk Mpango.

Alikemea tabia ya baadhi ya wafamasia kuiba dawa na kuwafanya wananchi kulalamika wakati serikali inatumia fedha zaidi ya Sh bilioni 17 kununua dawa kila mwezi.

“Lakini cha kushangaza baadhi yenu sio waaminifu mnaiba dawa na kuuza kwenye maduka yenu,” alieleza.

Aliwasisitiza kuzingatia viapo vyao vya maadili ikiwamo vyuo vinavyofundisha wafamasia kuzingatia weledi na umakini katika taaluma, lakini pia katika kukabiliana na usitishwaji wa huduma za wafadhili katika baadhi ya dawa serikali imetoa Sh bilioni 141.9 za ununuzi wa bidhaa za afya.

“Kutokana na uwekezaji huo wa dawa mnyororo wa ununuzi wa dawa na vifaa tiba umeimarika kwani  upatikanaji wa dawa umefikia wastani wa asilimia 89 huku malalamiko ya wananchi juu ya ukosefu huduma za dawa nchini ukipungua,” alieleza.

Alisema katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita serikali imeajiri wanataaluma wafamasia zaidi ya 650 na  kusisitiza serikali imeendelea kuhakikisha taaluma hiyo inakua ikiwamo wanataaluma 13,705 kusajiliwa na Baraza la Famasi hadi sasa.

Alitoa wito kwa Baraza la Afya kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala kushirikiana na Chama cha Wafamasia kuendeleza tafiti na kushirikiana kutatua changamoto za jamii haswa tafiti kuhusu miti na mimea ya asili inayojulikana kuwa tiba katika jamii zenye kutengeneza dawa kwa kutumia teknolojia ili kutibu magonjwa kwa ufanisi zaidi.

Aliagiza mamlaka ya serikali za mitaa kutenga maeneo maalumu ya miti au bustani maalumu zinazojulikana kama mimea dawa ili kuihifadhi na kuwarahisishia watafiti wa dawa kufanya tafiti kwa urahisi kama nchi za India na nyinginezo wanazofanya.

Alikemea wizi na upotevu wa dawa za serikali badala ya dawa muhimu kupatikana kwenye maduka ya dawa zinapatikana kwenye maduka binafsi.

“Mnaiba dawa na kwenda kuuza kwenye maduka yenu wakati serikali inanunua dawa ili wananchi wapate huduma, lakini baadhi yenu sio waaminifu mnaziiba na kupeleka kwenye maduka yenu binafsi. Mkibainika vyombo vya dola mchukue hatua,” aliagiza Dk Mpango.

Rais wa Chama cha Wafamasia Tanzania (PST), Fadhil Hezekiah aliiomba serikali kuwasaidia ili wawe na kituo cha pamoja cha ubunifu wa afya ili kuzalisha bunifu zenye tija na kuchochea ubora wa bunifu za bidhaa za afya ikiwamo uanzishaji viwanda.

Alisema wafamasia wataendelea kutoa huduma za afya, ikiwemo matumizi sahihi ya dawa ili kuepusha usugu wa vimelea vya dawa.

Pia, ameiomba serikali kuwasaidia muundo kuanzia Wizara ya Afya, hospitali za kanda, mikoa na wilaya ikiwamo rufaa kuwa na Kurugenzi ya Dawa ili kuwezesha upatikanaji wa dawa unakuwepo ili kuendana na uhalisia wa utoaji huduma bora za afya, ikiwamo muundo wa Ofisi ya Mfamasia Mkoa, Wilaya na Halmashauri.

Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Grace Magembe kwa niaba ya Waziri wa Afya, Jenista Mhagama alisema kada hiyo ni muhimu na ya kimkakati katika sekta ya afya.

Aliishukuru serikali kutoa kipaumbele katika sekta ya afya ikiwamo Sh bilioni 166.7 kupokelewa katika mwaka
wa fedha 2024/25, na sasa imetoa Sh bilioni 114.98 kwa bidhaa za afya kama dawa za Ukimwi, kifua kikuu na
dawa za watoto kujazilia pengo kutokana na mabadiliko ya utoaji dawa kupitia Serikali ya Marekani.