Matumizi sheria manunuzi yasisitizwa miradi ya ujenzi

KIGOMA: WAKUU wa Taasisi na vitengo vya ugavi na manunuzi katika mikoa ya Kanda ya Magharibi wametakiwa kutekeleza takwa la kisheria la kutumia asilimia 30 ya fedha zinazokwenda kwenye miradi ya ujenzi baadhi ya kazi kufanywa na vikundi vya kijamii. Katibu Tawala wa Mkoa Kigoma,Hassan Rugwa ametoa maagizo hayo mjini Kigoma alipofungua kikao cha siku …
KIGOMA: WAKUU wa Taasisi na vitengo vya ugavi na manunuzi katika mikoa ya Kanda ya Magharibi wametakiwa kutekeleza takwa la kisheria la kutumia asilimia 30 ya fedha zinazokwenda kwenye miradi ya ujenzi baadhi ya kazi kufanywa na vikundi vya kijamii.
Katibu Tawala wa Mkoa Kigoma,Hassan Rugwa ametoa maagizo hayo mjini Kigoma alipofungua kikao cha siku mbili cha viongozi hao kutoka mikoa ya Singida, Shinyanga, Katavi, Tabora na Wenyeji Kigoma kikao kilichoandaliwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA).
Rugwa amesema kuwa pamoja na sheria na taratibu za miradi ya ujenzi kutoa maelekezo hayo lakini bado miradi mingi inafanyika bila vikundi vya kijamii kunufaika na fursa hiyo ambayo lengo lake kuongeza mzunguko wa fedha kwenye maeneo ambayo miradi infanyika.
SOMA ZAIDI
Sheria ya manunuzi yatajwa wizi serikalini
Awali, Meneja wa PPRA Kanda ya Magharibi, Suma Mwanjwango alisema kuwa kikao hicho kimekuja baada ya mkoa Kigoma kuonekana uko nyuma katika kutekeleza sheria ya manunuzi ya umma katika utekelezaji wa miradi ya ujenzi sambamba na tenda za ununuzi serikalini ambapo bado vikundi vya kijamii havijafaidika na fursa hiyo.
Mwanjwango alisema kuwa mkutano huo wa siku mbili utatoka na maazimio ya hatua za kuchukua baada ya kufanya tathmini ya hali ilivyo sasa na changamoto inayojitokeza kushindwa kutekelezwa kwa utaratibu huo.
Akizungumza katika kikao hicho, Meneja wa Wakala wa barabara mkoa Kigoma (TANROADS) Mhandisi Narcis Choma alisema kuwa fedha kwa ajili ya asilimia 30 ya kuvipa vikundi kushiriki kwenye miradi ya ujenzi zipo lakini vikundi vingi vinavyoomba havijafikia vigezo vilivyoainishwa.