Makalla: Utekelezaji Ilani ya CCM, turufu uchaguzi mkuu

Habari Leo
Published: Jun 10, 2025 16:12:16 EAT   |  News

KILIMANJARO: KATIBU wa Halmashauri Kuu (NEC), Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Amos Makalla amesema utekelezaji wa Ilani na maendeleo yaliyofanywa na Serikali ya CCM chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan ni turufu kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu. Akizungumza na wananchi katika eneo la Himo Wilaya ya …

KILIMANJARO: KATIBU wa Halmashauri Kuu (NEC), Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Amos Makalla amesema utekelezaji wa Ilani na maendeleo yaliyofanywa na Serikali ya CCM chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan ni turufu kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.

Akizungumza na wananchi katika eneo la Himo Wilaya ya Moshi Vijijini mkoani Kilimanjaro leo Juni 10, akiwa katika ziara ya yake ya kujenga chama Makalla alieleza hayo akisisitiza Rais Samia amepeleka maendeleo kwa wingi na kuwafanya kutotumia nguvu kuyaeleza pale muda utakapofika.

Makalla amesema CCM inamuona Rais Samia ni karata muhimu sana katika uchaguzi huo kwani kwa kazi alizozifanya anaingia katika historia kuwa kiongozi aliyoongoza kwa kupeleka fedha za maendeleo zinazoacha alama ambazo zitakipa nguvu chama chao hapo baadaye.

Amesema Rais Samia ametekeleza mambo mengi kwa kugusa sekta tofauti ikiwemo maji, umeme, elimu, afya, miundombinu ya barabara na mengineyo aambayo yamefilisi ajenda za wapinzani.

Makalla amepongeza taarifa ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo iliyotolewa na Mbunge wa Jimbo la Vunjo, Dk Charles Kimei kwani ameenda kata kwa kata na kueleza hali halisi ya miradi na kuainisha kwa uwazi pale palipokuwa na changamoto.

Amesema baada ya kueleza mafanikio CCM ina wajibu wa kutatua changamoto na kukiri kupokea changamoto ya fidia kwa wananchi waliopisha ujenzi wa kituo katika eneo la Gona na kuahidi kulifikisha kwa Waziri wa Ujenzi, Abdallad Ulega kwa ajili ya kufanya tathmini ili waweze kupata stahiki zao.