Geita wapigia mstari tamko la wazee Yanga

Habari Leo
Published: Jun 10, 2025 15:18:17 EAT   |  Sports

GEITA: UMOJA wa Matawi ya wanachama wa klabu ya Yanga mkoani Geita wamesema wanaunga mkono tamko la Baraza la Wazee wa klabu hiyo walioagiza viongozi wasithubutu kupeleka timu Juni 15, 2025. Wanachama hao walikutana katika tawi la Yanga kata ya Nyawilimilwa na kukubaliana kuwa wanasimama na wazee na uongozi wa Yanga taifa kutaka majibu ya …

GEITA: UMOJA wa Matawi ya wanachama wa klabu ya Yanga mkoani Geita wamesema wanaunga mkono tamko la Baraza la Wazee wa klabu hiyo walioagiza viongozi wasithubutu kupeleka timu Juni 15, 2025.

Wanachama hao walikutana katika tawi la Yanga kata ya Nyawilimilwa na kukubaliana kuwa wanasimama na wazee na uongozi wa Yanga taifa kutaka majibu ya kuahirishwa mchezo yatolewe.

Mratibu wa Matawi ya Yanga mkoa wa Geita, Rajab Mohamed amesema wanachama wa Yanga Geita hawataki timu iende uwanjani kama majibu ya kuahirisha mechi ya Machi 08, 2025 hayajawekwa wazi.

Amesema mchezo huo namba 184, kati ya wenyeji Yanga dhidi ya Simba maarufu kama dabi ya Kariakoo haupaswi kupangiwa tarehe bila wadau wa soka kupewa ripoti ya uchunguzi wa kuahirisha mchezo.

“Hii Yanga siyo timu ya viongozi, ni timu ya wanachama, hii siyo timu ya kuokota ni timu ya wanachama, wanachama ndio wenye mamlaka yote juu ya hii timu”, amesema Rajabu.

Amesema Bodi ya Ligi Kuu ya Tanzania (TPLB) haipaswi kutumia ubabe katika kumaliza sintofahamu ya mchezo huu badala yake wanatakiwa kujitathimini na kuja na mfumo jumuishi wa kupata suluhisho.

Katibu wa Matawi ya Yanga mkoa wa Geita, Edmund William amesema wanachama wa Yanga Geita wanaendelea kuupongeza uongozi na wazee wa Yanga kwa kushikilia msimamo wa kutopeleka timu.

Amesema uamuzi wa huo uendelee ili kutoa somo kwa bodi ya ligi juu ya njia sahihi za kuendesha mpira wa Tanzania pasipo kuathiri timu moja badala yake kila timu inufaike na uongozi wa soka uliochaguliwa.

Msemaji wa Tawi la Yanga Nyawilimilwa, Nkanga Malima amesema majibu ya bodi ya ligi juu ya sakata la kuahirishwa mchezo uliopita ndio yatatoa fursa kwa wanachama wa Yanga kuelewa hatima ya mchezo.

Amesema dhamira ya Yanga siyo kulumbana na mamlaka za soka nchini bali kiu yao ni kuona haki inatendeka na mpira unachezwa bila makandokando.