CCM yaja na mambo 11 kukuza uchumi wa buluu

Habari Leo
Published: Jun 05, 2025 05:04:05 EAT   |  News

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema katika miaka mitano ijayo kitaielekeza serikali ifanye mambo 11 ili uchumi wa buluu uchangie maendeleo ya uchumi nchini. Katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2025-2030, chama hicho tawala kimeeleza kuwa kinatambua fursa za kiuchumi katika rasilimali za maji ikiwamo bahari, mito, mabwawa na maziwa, lakini fursa ya uchumi wa buluu …

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema katika miaka mitano ijayo kitaielekeza serikali ifanye mambo 11 ili uchumi wa buluu uchangie maendeleo ya uchumi nchini.

Katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2025-2030, chama hicho tawala kimeeleza kuwa kinatambua fursa za kiuchumi katika rasilimali za maji ikiwamo bahari, mito, mabwawa na maziwa, lakini fursa ya uchumi wa buluu haijatumika kikamilifu kuchangia katika maendeleo ya uchumi wa nchi.

CCM imeeleza itaielekeza serikali ijenge bandari ya uvuvi Bagamoyo Mkoa wa Pwani na ikamilishe ujenzi wa bandari ya uvuvi Kilwa mkoani Lindi.

Ilani imeeleza itaiagiza serikali iongeze fursa za masoko ya bidhaa za uvuvi na mwani ili kuwawezesha wavuvi na wakulima kuwa na uhakika wa masoko.

Pia, serikali itaagizwa iwezeshe upatikanaji wa mitaji/mikopo na vifaa kwa wavuvi na wakuzaji viumbe maji, vyama vya ushirika na wawekezaji kwa kushirikisha taasisi za kifedha.

Ilani imeleeza CCM itaiagiza serikali ijenge mabwawa ya ufugaji wa samaki na vizimba vya kufugia samaki baharini na kuanzisha vituo vipya vya ukuzaji viumbe maji katika Ziwa Tanganyika, Ziwa Nyasa na maeneo mengine ya nchi.

Chama hicho kimeeleza kitaagiza kuimarisha miundombinu ya uvuvi kwa kukarabati na kujenga mialo na masoko ya samaki ili kuongeza thamani na ubora wa samaki na kupunguza upotevu wa mazao ya uvuvi.

Pia, serikali itaagizwa iimarishe usimamizi wa uvuvi nchini ikiwa ni pamoja na kukamilisha uanzishwaji wa Mamlaka ya Usimamizi wa Rasilimali za Uvuvi.

Ilani imeeleza CCM itaiagiza serikali inunue meli za uvuvi zitakazowezesha kuvua eneo la bahari kuu ili kuongeza upatikanaji wa mazao yatokanayo na uvuvi kwa matumizi ya ndani ya nchi pamoja na kuongeza mauzo ya nje ya nchi.

Aidha, kitaagiza wavuvi wazalendo wajengewe uwezo wa kufanya uvuvi wa kisasa kwa kuwapatia mafunzo na nyenzo na sekta binafsi ihamasishwe kuwekeza katika sekta ya uvuvi, ikiwamo uzalishaji wa vifaranga bora kupunguza gharama za uzalishaji.

Ilani imeeleza serikali itaagizwa kuendeleza mpango wa ujenzi wa mashamba darasa ya ukuzaji viumbe maji katika halmashauri za wilaya ili kusogeza huduma za ugani na utoaji wa mafunzo kwa vitendo kwa wananchi katika maeneo hayo.

Pia, itaagizwa ianzishe programu maalumu ya kupandikiza rejesha na kujazilia samaki walio katika hatari ya kutoweka kwa lengo la kuendeleza zao la samaki kama nyenzo ya uchumi na lishe.